Thursday, March 9, 2017

MAMBO 5 YA KUFAHAMU KABLA NA BAADA YA KUINGIA KATIKA MAPENZI




Mambo_ya_kuzingatia_katika_mapenzi
Mafanikio katika mapenzi huhitaji maelewano , uwajibikaji na busara kubwa ili waliopo katika mahusiano waweze kweli kunufaika na penzi lao. Katika Makala hii tutaangalia mambo makuu 5 ambayo yakizingatia na kufanyika kwa ufasaha yanaweza boresha furaha na mafanikio katika mapenzi.
1. Utofauti kati ya  mahusiano, mapenzi na ndoa:
Ni muhimu kwa wapenzi kutambua  kama wanahitajiana, na kama kweli wanataka kuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu kabla ya kufikia hatua ya kula kiapo cha ndoa.
Ndoa ni kiapo mbele ya watu wengine , na ni namna ya kutaka kumuhakikishia mwenza wako kuwa endapo kiapo hicho kitatokea kuvunjika, basi unakubali rasmi kuwajibika kwa mujibu wa taratibu zilizopo za ndoa husika, ikiwemo kukubali kuitwa kwenye mabaraza ya usuluhishi, kugawana mali, n.k. Na kwa upande wa kiroho, inabeba maana zaidi kuwa unaweka kiapo kwa Mungu wako kuwa utalinda mahusiano yako na huyo unayemchagua.
Ndoa ni namna tuu ambayo wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu rasmi watu wengine kuwa wao wapo rasmi katika mahusiano. 
Hivyo basi, ndoa haijengi mahusiano wala mapenzi. Kiuhalisi inabidi kwanza yawepo mahusiano na mapenzi kisha ndio kiapo kifanyike, kwani kinyume cha hivyo ni kuwa unakula kiapo ‘feki’.
Kutumia ndoa kama kinga ya kuhakikisha mahusiano yako yanadumu ni maamuzi magumu ambayo pengine yanaweza yasilete faida hapo baadae. Au kuingia kwenye ndoa wakati tayari unaona mahusiano yenu tuu ni shida, ila unajiaminisha kuwa mwenza wako kwakua mkiwa kwenye ndoa na kwa sababu ya watoto basi atatulia na mtaishi tuu vizuri ni uamuzi mgumu ambao unawezakana usikuletee mafanikio.

2.Matarajio waliyonayo waliopo katika mapenzi
Kabla hata ya kuingia katika mahusiano na hatimaye ndoa wengi wetu huwa na matarajio binafsi ya kimaisha. Matarajio haya yanajumuisha vile tunavyotaka sie wenyewe kuwa hapo baadae, pamoja na matarajio ya vile tunavyotaka wenza wetu wawe.
Hata hivyo katika hali halisi tunajikuta sisi wenyewe hatuwezi kujibadilisha au kujiweka kwa usahihi vile tunavyotamani kuwa (kwa sababu kwa kila tunachojaribu kufanya kuwa bora, tunajikuta bado tuna madhaifu mawili matatu). Pamoja na ukweli huu wengi hutaka kuwabadili wapenzi wao wawe wa aina fulani hivyo kuishi Maisha ya matarajio ambayo ni magumu wakati mwingine.
Kwakuwa kiasili binadamu ni kiumbe huru, wenza wetu  huwa ‘busy’ kutimiza ndoto za vile wanavyotamani kuwa iwe kimavazi, aina ya marafiki, utafutaji wa kazi , kujiendeleza kimasomo, aina ya mali za kununua, hata kufikiria tofauti aina ya maisha wanayotaka muishi.
Matokeo yake ukinzani huu wa matarajio ni mkanganyiko wa mgongano wa mawazo kati ya wawili nyie, na mwanzo wa vita ya chini kwa chini ya nguvu ya maamuzi katika mahusiano yenu.
Ndio maana sio ajabu kuona wapenzi walioishi pamoja kwa miaka 15 wakiachana kisa ni kuwa mmoja wao amechoka aina fulani ya maisha au ametamani kuwa wa aina Fulani.

3. Kuweza kumbadili tabia mwenza wako
Ni bora uwe na subira uje upate mtu ambaye huhitaji kumbadili tabia au kumtengeneza awe vile unavyotaka wewe kwani unaweza badili muonekano na kumpatia vyote unavyodhani unaweza awe vile utakavyo lakini huwezi kumiliki uhuru wake wa maamuzi na kufikiria. Ipo siku atakuja kubaki yeye kama yeye na kufanya tofauti na vile ulivyokua ukitarajia kwani ulichofanikiwa wewe ni muonekano na kukubaliana kwa maneno na kwa matendo ila kiakili  na kimaamuzi bado kuna bomu linalosubiri kulipuka siku akiamua kuwa yeye kama yeye.
Na la kukumbuka ni kuwa wakati mwingine unaweza usisishinde kumbadili mtu kwakua tayari mtu huyo hajioni kuwa anaweza kubadilika, au ana misingi mingine ya Imani kuhusu hivyo alivyo au anavyopaswa kuwa kiasi kwamba kusikiliza usemacho Hata hivyo wengi wetu kwenye mahusiano, hutegemea ‘mapenzi’au vitisho tuu kama vile ‘nitakuacha mie ’,  kama sababu ya kumfanya mtu abadilike kitabia.Udhaifu wetu katika kutambua asili ya tabia ya mtu husika na mbinu za kisayansi za kubadili tabia hufanya zoezi la kubadilishana tabia kuwa gumu na pengine lisilowezakana.

4. Mtazamo wa kuvumilia katika mahusiano
Kusameheana ni jambo la asili, na tunapaswa kusameheana kwa mambo mengi nje hata ya mahusiano. Hata hivyo msisitizo mkubwa uliopo kuhusu kusameheana katika mahusiano kunafanya wengine waache kujiboresha ili wasikosee na kuwakwaza wenza wao, badala yake wanalalia zaidi katika ukweli kuwa wanatarajia kusamehewa.
Kila mtu analo jukumu la kufanya bidii kuwa mtu mwema, hivyo hauhitaji kubeba ‘uzembe’ wa mwingine kwa kisingizio tuu cha kuwa unaonyesha upendo hususani pale ambapo ni kwa uzembe tuu au kutokujali kwake mwenza husika amefanya jambo fulani.
Amini usiamini, kasumba hii ya kutarajia aina ya pekee ya kusamehewa na kuvumiliwa kwa kisingizio tuu cha kuwa upo kwenye mapenzi na mwenza wako, hurudisha nyuma maendeleo ya mahusiano yenu kwani mwenzi wako nae ni binadamu na kumbuka anayo matarajio mengine ya maisha, isitoshe na yeye anahitaji upendo na kujaliwa na wewe, hivyo kutarajia kwako kusamehewa na kuvumiliwa kunamnyima haki mwenza wako. Hatimaye kutegemea kwako kusamehewa kila wakati, kunamfanya mwenza wako atilie mashaka upendo wako kwake.

5. Uaminifu , Upendo na Kudumu kwa mahusiano
Pamoja na ukweli kuwa mwenza wako anatarajia utakuwa muanifu kwake, elewa kuwa kuwa mwaminifu pekee katika mahusiano yako sio tiketi ya kudumu kwa mahusiano yenu kwakuwa watu wanaingia kwenye mahusiano sio tuu kwa kuwa wanataka kuwa na mtu mmoja muaminifu bali wana mahitaji mengine wanayohitaji.
Zungumza na mwenza wako, fanya utafiti wako binafsi kuhusu mpenzi wako ujue mambo mengine anayohitaji toka kwako. 
Pia msikilize anapokutaka urekebishe mambo kadhaa au ufanye mambo fulani. Inapendeza pale unapomfanyia mtu mambo yanayompendezesha kwa kuwa hivyo ndivyo anavyotaka, sio kwakuwa tuu wewe unadhani kufanya hivyo kutampendezesha mhusika.
Upendo ni kujisikia kujitoa kwa ajili ya mwingine, ni kumfanyia mwenzako vitu anavyohitaji. Usipofanya vitu anavyohitaji ukawa wewe tuu unataka kufanya unavyodhani anahitaji au unavyopenda wewe hapo ni shida. Kumfanya  mwenza wako afurahie uwepo wako kila siku ndio kazi yako kuu katika uhusiano wenu.

Share this article :

0 comments:

Post a Comment