Wednesday, February 22, 2017

MWANAMKE KUJIAMINI: MBINU 5 ZA KUWA MWANAMKE MWENYE FURAHA SIKU ZOTE


Nimekua nikiongea na wanawake wengi ambao kwa mtazamo wa nje wanaonekana wana sifa zote za kuwa na furaha katika maisha, hata hivyo wanalalamika hawana furaha katika maisha yao.
Nasema kwa mtazamo wa nje wanaonekana kama vile wangekua na maisha ya furaha ni kwa sababu wengine wana kazi nzuri, wana nyumba nzuri na familia zinaonekana kustawi, wana kazi nzuri, wana elimu nzuri, ni wazuri wa sura na maumbo, ila bado hawana furaha katika maisha yao.
Kukosa furaha huku kumepelekea wengine kutokutaka hata kujipamba wala kujiweka nadhifu  eti kwa sababu kuna mtu alimsema kwamba yeye hana sura nzuri, hana umbo nzuri,  yeye siyo mweupe, siyo mrefu , hazai, amechelewa kuolewa, mwanaume amemuacha akaoa mwanamke mwingine au amezalishwa hakuolewa .
Katika makala hii ntakueleza mambo ambayo yatakufanya uwe mwanamke mwenye furaha maishani kila siku.

Amini  kwamba wewe ni wa kipekee:
Wewe ni  wa kipekee maana Mungu ameweka vitu tofauti tofauti ndani yako tofauti na mwanamke mwingine. Hata jinsi  tu ulivyo  Mungu aliona  unafaa kuwa hivyo na hakuna alichokosea wakati anakuumba,labda angekuumba kwa aina nyingine ungetisha na ndio maana upo hivyo ulivyo.
Amini  unaweza kufanya mambo mazuri na makubwa kuliko hata hao wanaokudharau au hao unaojaribu kuwaiga.

Jifunze kutatua matatizo unayokutana nayo uso kwa uso:
Unapopata tatizo fulani usianze kumwambia kila mtu badala yake fikiri sawa sawa namna gani waweza kukabiliana nalo. Ukiona  unashindwa kabisa basi tafuta ushauri kwa mtu  anayejiheshimu na mwenye hekima . Mtu ambaye anaweza kukushauri awe pia ambaye  unamuona  amefanikiwa katika eneo hilo ulilokwama.
Usijisemee  tu tatizo litaisha lenyewe au kuridhika na tatizo badala yake  tumia akili yako vyema . Usitafute njia rahisi kumaliza tatizo,tafuta kumaliza vyanzo vya matatizo unayokutana nayo.

Jiheshimu na uheshimu wengine  wakubwa  kwa wadogo:
Wakati mwingine unaweza kukosa furaha kwa sababu unahisi watu wanakudharau au haukubaliki, ila kumbe ni wewe tuu ndio ambaye unasababisha hao watu wakuchukulie hivyo.
Fahamu vile utaheshimu wengine ndivyo  utakavyoheshimiwa. Achana  na utani ambao haukujengi zaidi tu unakushushia heshima. Fikiria vizuri unayotaka kusema kabla hujasema , na epuka ugomvi.

Uwe na marafiki sahihi
Aina ya marafiki ulionao inaweza changia namna ambavyo wewe unayafurahia maisha yako maana hao marafiki wanaathiri vile wewe unavyoona maisha na kuchukulia mambo. Na usipokua makini kama marafiki zako ni watu wa kukata tamaa, watu wenye mitazamo hasi na wasiokupa moyo katika ndoto zako itakua ngumu kwako kuwa mwenye furaha.
Pia kumbuka hata kama umeambiwa jambo la kukuudhi au kukutatisha tamaa, nawe tumia akili zako kuchambua mambo. Usikubali uwe na marafiki ambao hawakusaidii kuiona furaha katika hayo unayotaka kufanya.
Katika hili la marafiki nigusie pia hata kuwa na mpenzi asiye sahihi nako kunaweza kukukosesha amani na furaha. Zungumza na mwenza wako kuhusu usiyoyafurahia, na kama ni wewe wa kujirekebisha , jihoji unawezaje kujirekebisha.

Fikiria kwa usahihi kuhusu uhusiano wako wa mapenzi:
Wanawake wengi hukosa raha wakiwa katika mapenzi kwakua hujiambia mambo ambayo huwakatisha tamaa au kuwafanya wajisikie wadogo. Mfano kuwaza kuwa pengine mwili wake si mzuri kama ambavyo mwanaume wake anahitaji, hii ni kwa sababu huyo mwanamke ameanza kujilinganisha na wanawake wengine pengine wenye matiti mazuri zaidi, au wenye makalio makubwa zaidi, au wenye rangi fulani tofauti.
Wakati mwingine kukosa furaha huja kwa kujilinganisha na wanawake wengine kielimu, au kiuwezo wa ajira, au mbona mwanamke mwingine hajazaa , au hana mtoto wa nje  hivyo kujishusha thamani.
Jitulize kama upo na mwanaume anayekupenda kweli yeye kaona vitu vya msingi kwako ndio maana yupo nawewe. Usiwaze mambo mengine kwani haupo kichwani mwa huyo mwanaume. Ni wewe na yeye ndio wenye majukumu ya kutunza penzi lenu. Jiboreshe katika mahusiano yenu, na utafurahia mapenzi yenu.

Hitimisho:
Tumeona katika maelezo hayo yoote, furaha ya kweli inategemea sana na wewe mwenyewe mhusika. Ni vile unavyotafsiri mambo yanayokutokea au yaliyokutokea maisha yako. Na vile unavyojiandaa kisaikolojia kujitambua na kukabiliana na mambo.
Anza kujiboresha katika fikra zako sasa, jiamini na jiendeleze katika kujiweka mwenye furaha siku zote.
Usiache kuendelea kusoma makala zaidi hapa hapa Tutunata Blog, utapata mambo mengi zaidi ya kukujenga kila siku.


Share this article :

0 comments:

Post a Comment