Friday, March 17, 2017

KWANINI MAZOEA HAYA NI ADUI WA MAFANIKIO YAKO


tabia_zilizo_adui_wa_mafanikio
Tumekuwa tukifanya mambo kwasababu tumezoea hata kama hatufaidiki tunafanya tu.
Na hii imetukwamisha maeneo mengi kama shuleni,kazini,mahusiano ,biashara, familia na hata kwenye nyumba za ibada.
Katika makala hii tutaangalia mazoea haswa mazoea mabaya yalivyo audi wa mafanikio yako na tutahitimisha kwa kuangalia namna gani unaweza kujikomboa kutokana na mazoea mabaya.

Kwanini ni rahisi kufanya mambo kwa mazoea
Ukishazoea kufanya jambo, basi jambo hilo huwa rahisi kwako kwani unaweza jisikia kama vile ni sehemu ya maisha yako. Jambo jipya ambalo hujalizoea huonekana gumu, na hivyo ni rahisi kwako kuona bora ufanye lililo rahisi yaani lile ulilolizoea.
Na ndio maana unapomwambia mtu inakubidi ubadilishe mfumo uliozoea kuutumia na utumie mbinu mpya kufanikiwa atakwambia siwezi nimeshazoea hata kama hicho kitu kinaathiri maisha yake hajali.
Vitabu vya dini vinasema kuna mtu jeshi lake lilikuwa likipigana vita na akaona usiku unaingia ,na haikuruhusiwa kupigana vita usiku. Akatamka na kusema jua na mwezi visimame navyo vikasimama . Akapigana vita na jeshi lake likashinda, alifanikiwa kwasababu aliona inawezekana kusimamisha mambo mengine hata kama siyo kawaida ili tu ashinde . Siyo kwa sababu ni mazoea usiku umeingia basi ameshindwa,Ila yeye alitafuta kushinda kwa namna yoyote ile ambayo ni halali.

Mazoea yanavyokudanganya
Tatizo la mazoea ni kuwa yanaweza kukufanya uamini kuwa wewe  ndivyo ulivyo hivyo na kuwa huwezi kufanya tofauti na hivyo. Mara ngapi umekua ukisema huwezi kufanya jambo fulani kisa tuu eti wewe upo hivyo. Unakubali kuwa mambo fulani yapo juu ya uwezo wako kwakua tuu hujawahi kufanya hayo mambo na kwamba hayo mambo ni kinyume na mazoea yako.
Angalia mifano hii jinsi mazoea yanavyowafanya watu wasifanikiwe:
-Hata mende wamekushinda akili  na kubaki ndani ya nyumba yako kwa maana wanatawala ndani ya nyumba yako unasema ni kawaida.
-Kucha,meno na vingine vingi umeshindwa kusafisha umeridhika unasema nimeshazoea tu kawaida tu.
-Huwezi mpelekea zawadi mume/mke na ukamkumbatia na kumwambia unampenda sababu umeshamzoea ni wa kawaida.
-Kuna aina fulani za nguo nzuri tu za heshima huwezi vaa sababu umeshazoea kuvaa unavyo vaa.
-Huwezi kufika nyumba ya ibada kwa muda uliopangwa sababu umeshazoea kuchelewa.
-Huwezi kupika chakula kwa namna nyingine kikawa na ladha nzuri zaidi sababu umeshazoea kupika mradi umepika.
- Hata ukisikia kuna mbinu mpya unazoweza kufundishwa kuboresha biashara yako,hutaki kwa sababu umeshazoea tu hivyo na unapata pesa inatosha.
-Unakuta mtu ana uwezo wa kununua anachotaka lakini ni lazima aombe mtu amnunulie kwa sababu ameshazoea kuomba omba.
-Huwezi kubuni kitu chako binafsi sababu umeshazoea kuiga iga.

Hatari Ya Mazoea Mabaya
Angalia Mazoea Yatakukwamisha Mengi katika maisha kama vile:
*Yatakutenga na watu ambao wangekusaidia.
*Yataazuia mafanikio yako.
*Mungu hawezi kukubariki ikiwa unafanya vitu kwa mazoea bila kumaanisha.
*Huwezi kwenda mbali kwa kufanya vitu kwa mazoea.
*Hata afya itakuwa ya mgogoro sababu tu ya mazoea
vunja mazoea na utafute kuwa bora zaidi na kufanya mambo kwa ubora zaidi.

Unaanzaje kubadilika ?
Kama ilivyo mazoea mabaya huwa sehemu ya maisha yetu na kutufanya tujisikie sisi ni kama vile tulizaliwa tupo hivyo, nakualika leo uanze kujizoesha mambo yaliyo bora. Najua kuanza itakua ngumu ila utakapoweza kurudia mara kwa mara basi utaweza kujenga mazoea mazuri na hapo utakua mtu bora.
Tumia uwezo wetu binadamu wa kubadilika na kuzoea mambo kufanya uwe na mazoea mazuri na utafanikiwa.
Kila la kheri. Soma zaidi mambo ya maisha na mafanikio katika ukurasa wetu wa Facebook; www.facebook.com/tutunatablog. Bofya hapa ku like ukurasa wetu.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment