Wednesday, March 22, 2017

JITAMBUE: FAHAMU MTAZAMO UTAKAOUKUPA MAFANIKIO KATIKA MAISHA YAKO


Tembo wa kufugwa  na fundisho kuhusu mitazamo ya mafanikio

Katika maisha huwa tunapambana na mambo mengi ukiacha ya nje ya sisi wewe kama vile hali ya kiuchumi, elimu na siasa, kuna mapambano ambayo huwa tunayo ndani yetu ambayo bila mtazamo sahihi, kupata mafanikio ni ngumu.
Katika makala hii tutatumia mfano wa tembo wa kufugwa anavyobadilishwa mtazamo na kujiona hana nguvu. Soma vizuri mfano huu ili ujue unajipangaje katika kutumia nguvu zako ambazo leo huzioni hivyo unashindwa kuzitumia fursa zilizopo machoni pako.

Mfano wa tembo wa kufugwa
Tembo ni mnyama mkubwa sana,  anaweza hata kupindua gari, anaweza haribu nyumba na kufanya madhara makubwa tuu akiamua. Hata hivyo si ajabu kukuta tembo akiwa amefungwa kwenye kamti tuu na kamba au mnyororo wa kawaida kiasi kwamba kama akiamua kutumia nguvu zake anaweza kujinasua kutoka hapo alipofungwa.
Hata hivyo tembo wengi wa kufugwa hulazimishwa toka wakiwa wadogo kuamini kuwa wao hawana nguvu ya kujinasua toka sehemu walipofungwa.
Kinachofanyika kwa tembo hawa wa kufugwa ni kuwawekea vizuizi vikali toka wakiwa wadogo kabisa. Wakati huo wadogo kweli watajitahidi kwa nguvu zao kutoroka ila vizuizi wanavyowekewa huwazidi nguvu hivyo hubaki hapo hapo. Masikini tembo hawa hali hiyo huwafanya waamini hata wakiwa wakubwa kuwa hawawezi kujinasua hivyo si ajabu katika sehemu nyingi wanazofuga tembo kwa matumizi binafsi huwa wanaweza kuwafunga tuu tembo kwa mnyonyoro au kamba ambayo inaonekana ni rahisi kutoroka ila tembo hatofanya juhudi yoyote ya kutoroka.
Je wewe nawe ni kama huyo tembo wa kufugwa ?
Kila binadamu ana nguvu kubwa ambayo Mungu kaiweka ndani yake. Hata hivyo pengine wewe hujagundua au kuanza kuzitumia nguvu zilizopo ndani yako kwa sababu kama tembo wa kwenye mfano hapo juu, haujioni kuwa una uwezo wa kufanya hivyo.
*Nimekuambia story hii kwakua kama walivyo tembo, pengine na wewe kuna kitu umeaminishwa kutokana na maisha yako ya hapo kabla.
*Pengine ni kutokana na mazingira uliyokulia, kazi yako, elimu yako, marafiki na mwenza wako katika mapenzi, umekaa ukiamini kuna mambo huwezi kufanya.
*Umeruhusu kutokufanya mambo kwa sababu tuu unadhani huwezi, kwa sababu hapo kabla ulijaribu ukashindwa, kwa sababu watu wengi wamekufanya ujione wewe huwezi.
*Amka leo, jiulize je ni mangapi uliwahi kuwaza huwezi ila leo umeweza ? Kwanini hilo lingine unalosema hauwezi  libaki tuu kuwa haliwezekani ?
*Kumbuka #mafanikio huanza na namna akili yako inavyochukulia mambo. Vile unavyowaza ndivyo utakavyokua. Jione kwanza mshindi, jione kwanza kweli wewe ni wa kufanikiwa.
*Ili uweze kubadili maisha yako, inabidi kwanza wewe mwenyewe ujibadili, na hakuna njia bora ya kujibadili kama kubadili kwanza mitazamo yako haswa mitazamo ya kutokuweza.  
*Kumbuka akili yako ni chombo chenye nguvu sana, anza leo, ijaze akili yako na vitu chanya, ijaze akili yako vitu ambavyo vinawezekana.
Ufanye nini ujikomboe toka minyororo uliyopo ?
Kumbuka kile unachokipa nguvu  katika akili yako, ndicho kitakachokutawala, na ndicho kitakachokufanya uwe vile utakavyokuwa.
Usiogope kwamba watu watakushangaa kwani hawajawahi kuona uwezo wako mkubwa. Sote tuna uwezo mkubwa sana, mara nyingi wengi huwa hawautumii kwakua kama wewe vile umejiona hauwezi.

Share this article :

0 comments:

Post a Comment