Thursday, May 10, 2018

JINSI YA KUWA MTU MWENYE KUJIAMINI


Kutokujiamini ni janga kubwa kwa mtu binafsi na kwa wale wanaomtegemea. Kutokujiamini kunakufanya ushindwe kupiga hatua katika Maisha yako na wakati mwingine usiwe mtu mwenye furaha. Kutokujiamini hutokea katika maeneo mbalimbali iwe kwenye elimu, kazi , mahusiano, biashara, na hata malezi. 
Ili kupambana na kutokujiami na wewe uanze kuwa mtu wa kujiamini  inakupasa kwanza ujue kwanini haujiamini. Hivyo tuangalie sababu zifuatazo za kitaalamu kwa nini watu hupoteza kujiamini:
1.Kutokua na Uhakika wa namna ya kufanya  jambo husika: Unapokosa taarifa sahihi kuhusu kile ukifanyacho au kushindwa kuchanganua mambo vizuri utaanza kujitilia mashaka wewe mwenyewe na hivyo utashindwa kulifanya jambo husika.
Mfano kama hujui vema miundo ya sentensi za Kiingereza, huzijui kanuni na maneno ya English, utakapohitajika kuongea au kuandika kitu kilichonyooka, wewe mwenyewe utaanza kujitilia mashaka, uoga utaingia na utakosa kujiamini.
DAWA YAKE: Dawa ya kutokujiamini kwa sababu  huna uhakika na namna ya kufanya jambo ni kuhakikisha tuu unapata taarifa na ujuzi sahihi. Tafuta kujifunza na sana sana upate mtu atakayekuongoza na kusimamia maendeleo yako ya karibu ili akupe mrejesho vile unavyoendelea katika kujiboresha.
La kusisitiza hapa ni kuwa uwe tayari kupata ujuzi na kujiboresha ili uweze kujiamini kweli kweli.
2. Yaliyokutokea zamani kuhusu kushindwa jambo husika:
Wakati mwingine ni sehemu ya ubongo wako inayohifadhi mambo yaliyokutokea hapo awali ndiyo inayokufanya ukose kujiamini. Kumbukumbu ya wewe kushindwa jambo Fulani au kuabika kuhusu jambo hilo kunaweza kukupelekea kujitilia mashaka uwezo wako wa kulifanya hilo jambo sasa. Matokeo yake ni kutokujiamini.
DAWA YAKE: Jiboreshe ufahamu wako kuhusu Maisha kwa ujumla. Fahamu kuwa yaliyokutokea mwanzo sio lazima yakutokee tena. Muda umepita na wewe umekua mtu mpya, hivyo kushindwa mwanzoni kusikufanye ujione uliyeshindwa au utakayeshindwa siku zote. Angalia maboresho katika Maisha yako ambayo tayari umeyafanya. Jipe moyo na mtegemee Mungu ili uwe na uthubutu wa kufanya tena ukiwa mtu mpya na bora Zaidi.
3.Kutokua na maandilizi na maboresho ya mara kwa mara:
Kuna wakati hata lile jambo ulilowahi kulifanya hapo kabla na ukaliweza, inakutokea eti leo haujiamini kuwa utaweza kulifanya. Hii inatokana na maandalizi na kutokujifanyia maboresho ya mara kwa mara. Kujiamini ni jambo ambalo linahitaji kulelewa na hivyo basi jizoeshe kujiboresha mara kwa mara. Kkiama ilivyo kiota kinachojengwa kwenye tawi dhaifu, hakitokuwa bora, hivyo hivyo nawe usipokuwa na maandilizi na maboresho mazuri utakosa kujiamini.
DAWA YAKE: Kama kutokujiamini kwako kunatokana na kushindwa kujiboresha vema, basi jiwekee mkakati sasa wa kujiboresha katika yale ambayo ulishawahi kufanya kabla. Maandalizi bora ni muhimu hata kwenye kuongea mbele za watu tunasisitizwa sana kufanya maandalizi kabla ya kuenda kuongea mbele za watu.
4. Kujilanganisha na wengine na ushindani usio na lazima
Ni ukweli ulio wazi kuwa sote tunaishi au tulipo sivyo ambavyo tulitarajia au kutazamia miaka 10 iliyopita. Hii ina maana kuwa mambo hubadilika mara kwa mara na hakuna bingwa wa Maisha. Hivyo basi acha kujilinganisha na kujishindanisha na watu wengine.
Kujilinganisha na wengine na kutaka ushindani na watu vinatajwa kuwa ni adui wakuu wa kujiamini. Inawezekana kwa mfano hata kuongea Kiingereza unashindwa kujiamini kisa tuu unafikiria utakachoongea hakitokua bora kama cha Fulani. Unajilazimisha uongee kama mmarekani. Umejibadilisha sauti ili uongee sijui kama mdada gani mtangazaji wa redio.
DAWA YAKE: Ishi Maisha yakow ewe kama wewe. Kama ni kujiweka bora au kufanya jambo Fulani lifanye kwakua wewe kama wewe unataka hilo na sio kwa sababu wengine wanataka au unataka kuwakomesha au kuwalingishia wengine.
Ni kweli kuwa unapaswa kuwaangalia wengine wanafanya nini na wanajiboreshaje, lakini isiwe kwakua unataka kuwa kama wao au kuwapita maana haujui wao kwanini wanafanya wanayoyafanya, na wala hujui wapo katika hali gani ya Maisha. Isitoshe wewe unachokiona ni kile cha nje tuu, hujui wanapitia nini katika Maisha yao halisi.
5.Kujitegemeza Kupita Kiasi
Unapojiruhusu kusubiri kufanyiwa mambo mengi au kumuangalia mtu Fulani kama ndio mwenye uwezo wa kulifanya jambo matokeo yake ni kuwa wewe mwenyewe unajishusha chini, na mwisho wa siku ni kujiona wewe kama wewe hauna uwezo wa kufanya mambo kwa ufanisi nah apo ndipo kutokujiamini hutokea.
DAWA YAKE: Dawa ya kutokujiamini kwa sababu unamtegemea sana mtu ni wewe mwenyewe kuanza sasa kupenda kujifunza vitu na kuvifanya. Usipende urahisi rahisi, au kuwa mvivu kwakua yupo anayeweza kukufanyia mambo hata kama ni mpenzi wako au mtoto wako.
Watu wengi wamejisahau sana utakuta mambo mengi ni marahisi ila eti mpaka baba arudi, au mpaka mtoto aje amfanyie. Na sio kwamba hawezi ila keshajiona yeye keshapoteza kujiamini kwakua kaegemea sana katika kusubiri wengine wafanye.
6. Mazingira na watu ulionao karibu
Watu ulionao karibu au mazingira uliyomo yanaweza pia kukufanya ukakosa kujiamini. Kuna watu wao hupenda kukosoa sana na kuwafanya wengine walionao karibu wajione hawawezi. Watu hawa wanaweza kuwa hata wazazi, wapenzi wetu, mabosi wetu wengine mashoga na marafiki zetu.
Mazingira uliyopo pia yanaweza kukutengenezea viwango vya namna ya kuishi, au kukutengenezea matarajio fulani kiasi kwamba nawe ukijiangalia ni kama vile haujafikia viwango hivyo au unajiona huwezi kufikia.  Hii inaweza kutokea hata kwa mfano  yale unayosikia kuhusu kuishi na mpenzi wako. Nawe ukapoteza kujiamini mbele ya mpenzi wako kisa tuu wengine wameongelea mambo makubwa ambayo wanayofanya ambayo wewe kama wewe unahisi huwezi kufanya.
DAWA YAKE: Kaa mbali na watu ambao wanajiona wao ndio wajuaji na hawakupi moyo wa wewe kama wewe kufanya vile uwezavyo.
Kuwa makini na makundi , pamoja na utakachosikia mwisho wa siku fahamu wewe unayo Maisha yako na una misingi yako ya Maisha, na kwamba sio lazima ufanye yale ambayo wengine hufanya.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment