Friday, January 27, 2017

MBINU KUU YA KUJIEPUSHA NA MATATIZO MAKUBWA MAISHANI

No comments:
Wengi wana vilio mambo yamekuwa magumu,wamejaribu kutatua imeshindikana. Wengine dua na wengine wamefanya maombi  lakini bado mambo ni magumu.
Wengine wameishia kujilaumu na kulaumu wengine na kuna watu wamekata tamaa kabisa ya maisha na kuridhika na hali halisi kusema ni kawaida lakini siyo kweli.
Matatizo makubwa kwa watu na hata ulimwenguni  hayakuanza yakiwa makubwa,yalianza yakiwa madogo dogo tu na yakapuuzwa, si unajua hata mbuyu ulianza kama mchicha, na misemo mingi tu kama kama mdharau mwiba mguu huota tende. Ngoja nikuhadithie kisa kimoja kidogo:

Kulikuwa na shujaa mmoja mwenye nguvu sana.Siku moja katika mizunguko yake akatobolewa na mwiba,alipata maumivu makali sana akakaa chini akautoa.Baada ya kuutoa akashangaa! kamwiba kadogo kamemtesa hivyo , akachukia   akaurudishia na kuupigilia kabisa na nyundo.Alifanya hivyo kwa kujiambia hivi, shujaa kama mimi siwezi sumbuliwa  na kamwiba kadoogo hivi.Basi siku zikaendelea kwenda mguu ukaendelea kuvimba mwisho mguu ulioza na ikabidi akakatwe mguu.

Hapa tumeweza kuona tu kwa kifupi vile matatizo yanavyoanza na watu wanayapuuza kwa vile wanayaona ni madogo tu na wanafikiri itatokea tu yataisha yenyewe,siyo kweli hakuna tatizo linaweza kuisha lenyewe bila kutafutiwa ufumbuzi na mhusika mwenyewe.



HEBU TUANGALIE MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA KUTATUA TATIZO KABLA HALIJAWA KUBWA
-Ona vile linaweza kuleta madhara makubwa baadae.
-Usijidanganye utavumilia tu jiulize unaweza kuvumilia kwa muda gani?
-Kubali kuteseka ili tu kumaliza tatizo kabla halijakuwa kubwa.
-Fikiri vizuri je usipolitatua leo utalitatua lini?
-Watu wanaweza wasikuelewe wakati unapambana kutatua tatizo dogo leo lakini baadae watakuja kukuelewa.
-Acha kufa na tai shingoni kubali kwamba wewe ni sehemu ya tatizo na kwamba kulitatua tatizo hilo  ni bora kuliko kujionyesha mshindi wakati kiukweli una tatizo.

NIMALIZIE NA MFANO HUU.
Mtu anaanza uhusiano na mdada flani ambaye anamuona kabisa ni mvivu ama ni mchafu  ,badala amwambie mapema kabla hawajaingia kwenye ndoa, eti ananyamaza anasema nikimuoa atabadilika.Matokeo yake wanaowana ndiyo anakuwa mchafu zaidi tayari tatizo limeaanza kuwa kubwa,mume anaogopa kuleta hata marafiki zake nyumbani maana ni aibu. Matokeo yake mume anaanza kulewa na hakuwa mlevi ili tu akirudi asiuone huo uchafu,mara anatafuta mwanamke mwingine msafi ili ajifariji.
Anaanza kumsema mke wake kwa watu wa nje na marafiki Kwamba mkewe hafai lakini unashangaa kwanini si alichagua mwenyewe? Si alimpenda mwenyewe?


Hapo  ndio tunarudi na kusema usidharau tatizo au jambo ambalo unaliona dogo leo limalize mapema ama ujiandae kabisa kupambana nalo badae kama utaweza.
Continue Reading...

Saturday, January 14, 2017

KINYWA CHAKO KAMA CHANZO CHA MAFANIKIO MAISHANI

No comments:

Mungu amemuumba mwanadamu na kumpa kinywa ili aweze kula chakula aishi na aweze kuwasiliana kupitia kinywa hicho, ila wengi wetu tumekuwa tukitumia tofauti na baadhi wanatumia vizuri.
Yale unayosema yatakutambulisha wewe ni nani na maneno yako yatakuunganisha na watu wa aina yako.Pia maneno yako yanaweza kukutenga na watu au kukuunganisha na watu.
Na kuna watu wameshindwa kufanikiwa sababu ya midomo yao,siyo lazima kuongea ikiwa huna kitu cha kusema. Usiongee tu sababu unataka kuongea.

Jiulize haya kabla hujaongea;
-kwa nini unataka kusema hayo unayosema?
-Watu watafaidikaje na hicho unachosema?
-Watu watakuelewaje baada ya kukusikia?-
-Je ni muhimu sana kusema hicho unachosema kwa wakati huo na mazingira hayo?
-Wewe binafsi utapata faida gani na hicho unachosema?
-Na ukiona haina ulazima wewe kuongea nyamaza.
-Jiulize mbona wengine hawasemi na wewe ndio unataka kusema?

Sikia hiki kisa  kuna kitu nataka ujifunze:
Kuna mwanamke mmoja alienda kwa mganga, akitaka mganga ampe dawa amuwekee mume wake maana mume wake alikuwa akichelewa kurudi nyumbani,anarudi amelewa na mke anapojaribu kumwambia mbona anafanya hivyo alikuwa akimpiga.basi mganga akamsikiliza yule mwanamke akagundua yule mwanamke anaongea sana.
Basi mganga akafikiria ni jinsi gani ataweza kumsaidia huyu mwanamke ili apunguze maneno mengi ambayo ndiyo yanampelekea mume wake kurudi usiku,huku amelewa ili asimsikie akiongea.Mganga akampa yule mwanamke majivu akamwambia hiyo ni dawa,jinsi ya kutumia sasa akamwambia afanye kazi zake mapema kabisa akimaliza aoge na kujipaka hiyo dawa kidogo mikononi na usoni kidogo ahakikishe haionekani na amsubiri mumewe,mumewe anaporudi amkumbatie na ,amshike na ile mikono aliyojipaka dawa na kumbusu na kumwambia anampenda .Baada ya hapo amtengee maji ya kuoga  akimaliza kuoga basi ampe chakula.Wanapofika kitandani ampe mapenzi motomoto.Na ikiwa atamwongelesha mumewe maneno mengi au kwa ukali basi dawa ingeharibika.Mwanamke akafanya kama alivyoagizwa na mganga mume akashangaa mbona mkewe haongei sana kama mwanzo?siku ya kwanza, ya pili , ya tatu mume akaacha pombe akaanza kuwahi nyumbani na ndoa ikawa na Amani.Akarudi kumshukuru mganga akamwambia maneno yake mengi ndiyo yaliyokuwa yakiharibu ndoa yake,basi yule mwanamke akajifunza kwamba namna  gani anafaa kuzungumza na mumewe.

Turudi kwenye mada yetu.
-Siyo lazima useme kila unachokiona au unachoambiwa au unachosikia.
-Usiseme habari za mtu ambazo hajakutuma kusema.
-Usifikiri watu walionyamaza hawazungumzi hovyo labda hawajui unachokijua au hawaoni unachokiona.
-Hakikisha unasikiliza Zaidi kiliko kusema.
-Usipende kuzungumzia jambo usilolijua vizuri maana hii itawafanya wanaokusikiliza wakudharau.
-Sema ukweli.

KUMBUKA HII SIKU ZOTE.
Mpumbavu akinyamaza katikati ya wenye hekima naye huhesabiwa pamoja na wenye hekima.
Continue Reading...

Friday, January 13, 2017

HATUA 3 ZA KUBADILI TABIA INAYOKUKWAZA

1 comment:

Kati ya kitu ambacho kinasumbua wengi na kimekwamisha wengi ni tabia.Wengi wana huzuni ndoa zimewashinda,kazi zimewashinda,fedha na mafanikio vimewakimbia,watoto wamewashinda,hawana marafiki hata miili yao haina afya kwa sababu ya tabia tu.
Wengine wamejiona ni kama wana laana,wengine wanafikiri labda wanaugua ugonjwa flani lakini shida siyo shida nitabia zao tu.
Hebu tuone namna gani tunaweza badilika au kubadilisha tabia zetu.

Tafuta Kujijua Binafsi:
Jiulize kwa nini umekuwa ukikwama mara kwa mara katika eneo  flani kama vile:-
(a)Kwanini haudumu ktk mahusiano ya kirafiki au ya mapenzi.
(b)Kwanini umeshindwa kufanikiwa kimaisha.
(c)kwanini watu wanakuchukia.
(d)kwanini hau-dumu kwenye kazi.
Unaweza pia kumuuliza mtu unaye mwamini akwambie jinsi ulivyo.

Jione Kwamba Unahitaji Kubadili Tabia:
Kubali binafsi kwamba haukuwa ukifanya vizuri kwa kuzingatia yafuatayo:-
(a)Chukia hiyo tabia.
(b)Ona jinsi imekukwamisha mambo mengi.
(c)Usiogope kwamba watu watakucheka au watasemaje sababu hapa unahitaji mabadiliko na ukumbuke ni wewe unaumia na siyo watu.
(d)Hata kama utaumia na kuteseka vumilia tu maana unatengeneza kitu kizuri.
(e)Usiwe mbishi kubali kukosolewa na kuonywa bila kukasirika na usiwe wa kujitetea sana.
(f)Kubali kuambiwa ukweli hata kama unauma na usikasirike.

Chukua Hatua Kubadili Tabia:
Anza kufanya kinyume na ulivyokuwa umezoea kwa maana ya kwamba yale ambayo ni mazuri sasa. Zingatia haya:-
(a)Wataalam wa mambo wanasema ili jambo liwe tabia linafaa kufanya kwa siku “21” bila kuacha  baada yah apo jambo hilo litakuwa tabia.
(b)Ikikubidi kubadilisha mazingira ambayo unahisi ndiyo yamekuharibia tabia badisha hata kama itakugharimu.
(c)Ikikubidi kubadili marafiki ambao wamekuwa wakikushauri vibaya achana nao tu utapata marafiki wengine.

Majumuisho
Kumbuka haya:
(a)Tabia inaundwa au inatengenezwa na tabia ya mtu inamtegemea mtu mwenyewe na maamuzi yake.
(b)Tabia yako inaweza kukukwamisha kabisa katika Maisha yako yote au kukufanikisha katika mambo yote.
(d)Tabia yako itakutenga na watu au itakuunganisha na watu.
SASA UAMUZI NI WAKWAKO KUTENGENEZA TABIA YAKO ILI WATOTO WAKO WAIGE MEMA KUTOKA KWAKO.

Continue Reading...